Mmoja
wa wakunga wa jadi Bi. Namboto Sheha Kombo akielezea jinsi wanavyofanya
kazi zao za ukunga katika mkutano uliofanyika Hospitali ya Kivunge Mkoa
wa kaskazini “A” Unguja.

Naibu
Waziri wa Afya Zanzibar Mahamoud Thabit Kombo akizungumza na wakunga wa
jadi, na kuwataka washirikiane na watalaam wa Afya katika kazi zao ili
kupunguza vifo vya Akinamama na watoto.

Msaidizi
daktari dhamana Hospitali ya Muembe ladu Ruzuna A.M. Shamte
akifahamisha kitu katika mkutano wa wakunga wa jadi na watalam wa afya
huko Kivunge Mkoa wa kaskazini “A” Unguja.
Baadhi
ya Wakunga wa Jadi na watalam wa Afya waliofika katika mkutano wa
kukuza mashirikiano huko Kivunge Mkoa wa kaskazini “A” Unguja
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mahamoud Thabit Kombo
(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.

Dkt.
Dhamana Hospitali ya Kivunge Khamis Hamad Ali akitoa nasaha zake katika
mkutano wa Wakunga wa Jadi na watalam wa Afya wa kukuza
mashirikiano katika kufanya kazi zao. Picha na Makame Mshenga- Maelezo
Zanzibar.
…………………………………………………………………………………….
…………………………………………………………………………………….
Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar
Dawa za Kienyeji wanazopatiwa kina
mama wajawazito kutoka kwa Wakunga wa Jadi wakati wa kujifungua
husababisha matatizo ya kiafya kwa watoto wanaotarajiwa kuzaliwa pamoja
na akina mama hao.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa
Afya Zanzibar Mhe. Mahamoud Thabit Kombo wakati akizungumza na Wakunga
wa Jadi wa Vijiji vya Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja katika ukumbi wa
mikutano wa Hospitali kuu ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyopo katika
kijiji cha Kivunge mkoani hapo.
Amesema kuwa dawa hizo hua
zinahatarisha zaidi maisha ya kina mama wajawazito na watoto
wanaotarajiwa kuzaliwa hususan kwa akina mama wenye viashiria hatari
wakati wa ujauzito ikiwemo maradhi ya Presha na Sukari ambayo yanaweza
kusababisha kupoteza uhai wao kwa haraka zaidi.
Naibu Waziri huyo amesema ipo haja
kwa Wakunga wa Jadi kuwafikisha kina mama wajawazito katika Vituo vya
Afya pindi wanapobaini kuwa kina mama hao wana matatizo ya kiafya au
mtoto kuleta matatizo wakati wa kujifungua na kuacha kung’ang’ania
kuwazalishia nyumbani ili kuokoa maisha ya mtoto na mama mja mzito.
Kwa upande wake Daktari Dhamana wa
Hospitali ya Kivunge Nd. Khamis Hamad Ali amesema ipo haja kwa Wakunga
wa Jadi kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar ili kufanikisha zoezi la
uzalishaji wa kina mama kwa usalama zaidi pamoja na kuwaomba Wakunga
hao kwenda nao wagonjwa katika vituo vya afya kwa kupata uangalizi wa
kitaalamu zaidi.
Amesema watoto wengi hupata
matatizo ya magonjwa yakiwemo ya Kifafa na Utaahira kutokana na uchungu
mkali unaowapata kina mama wakati wa kujifungua hususan kwa wale
wanaojifungulia kwa Wakunga wa Jadi kwani wakunga hao huwa hawana vifaa
vya kupunguza makali ya uchungu wa kina mama hao ikiwemo sindano maalum
wanazochomwa kina mama kwa ajili ya kupunguza uchungu huo.
Sambamba na hayo Dkt. Khamis
amesema inaripotiwa kuwa 5% – 15% ya wanawake wote Duniani huwa wanapata
matatizo wakati wa kujifungua pamoja na kuwaomba kina mama kuwa wawazi
kuelezea matatizo waliokwisha kuyapata kabla ya siku za kujifungua
kufika pindi wanapokwenda katika vituo vya afya ili kurahisisha
uzalishaji huo.
Nae Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya
Muembe Ladu Zanzibar Dkt. Ruzuna Abdulrahman Moh’d amesema ipo haja kwa
Wakunga wa Jadi kupatiwa Taaluma na Elimu ya kisasa ili waendelee
kuisaidia Serikali kwa kuwazalisha kina mama wajawazito kwa njia za
kisasa na zilizo salama zaidi.
Ametanabahisha kuwa dawa za
kienyeji zinaweza kutumika kwa kina mama waliokwisha kujifungua ikiwa
mtoto amezaliwa bila ya matatizo yoyote ya kiafya.
Nao Wakunga wa Jadi wa Wilaya
Kaskazini “A” Unguja wamesema kuwa akina mama wengi waja wazito huwa
wanakimbia kwenda kuzalia Hospitali ili kukimbia manyanyaso wanayoyapata
kutoka kwa madaktari hususan kutoka kwa madktari wadogo na hivyo
kuwaomba madaktari hao kujirekebisha kitabia ili kuokoa maisha ya kina
mama na watoto kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha wamewaomba madaktari kutoka
serikalini kuendelea kutoa elimu ya uzazi kwa akina mama na Wakunga wa
Jadi pamoja na kuwaasa wananchi wenzao hususan kina mama kwa
kuyasikiliza na kuyafanyia kazi yale yanayotolewa na Wataalamu wa Afya
kwa lengo la kujiongezea ujuzi katika kazi yao ya uzalishaji wa akina
mama.
0 comments:
Post a Comment