![]() |
Wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, wakimshangilia Juma Duni Haji (aliyevaa
kanzu) nje ya ukumbi wa bunge baada ya mjumbe huyo kuwalisilisha bungeni
maoni ya waliowachache ya Kamati namba11. Picha: Mwananchi |
Dodoma. Shamrashamra za wajumbe wanaounga
mkono serikali tatu na mbili, nje ya Bunge jana, ziliendelea baada ya
Mjumbe, Juma Duni Haji kutoa ufafanuzi wa kutetea serikali tatu na
kuwavutia wajumbe, ambao walitoka ukumbi wa bunge wakimshangilia babu,
babu, hawatuwezi hawatuwezi.
Tukio hilo ambalo ni mfululizo wa
vijembe, baina ya wajumbe wa CCM na upinzani, kuhusu hoja ya serikali
tatu au mbili, lilisababisha viwanja vyote vya bunge jana mchana,
kutawaliwa na kelele za kushangilia na kuzomeana.
Akitoa ufafanuzi wa kamati namba 11, Duni
alisema siyo serikali tatu ni ufumbuzi wa malalamiko ya Muungano,
ambayo yanaifanya Zanzibar kuendelea kubanwa na kushindwa kuwapatia
maendeleo wananchi wake.
Alisema serikali iliyopo madarani kwa
miaka 50 sasa, imeshindwa kutumia rasilimali zilizopo Zanzibar na
kuifanya iwe kutovu cha utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati
badala yake inazuia kila jambo jema la maendeleo.
“Kama mngekuwa na dhamira ya dhati na
Zanzibar, leo Zanzibar ingekuwa kama Hong Kong ya Afrika lakini hakuna,
Zanzibar imefungwa mikono na miguu hata kutembea haiwezi,” alisema.
Alisema hoja kuwa katika muundo wa
serikali tatu, ukianza Zanzibar haiwezi kuchangia Muungano siyo ukweli
kwani, uchumi wa wananchi wa Zanzibar hauna tofauti na uchumi wa
Watanganyika kwa mtu mmoja moja. Akizungumzia takwimu za tume ya
mabadiliko alisema zipo sahihi kuwa waliotaka Muungano wa Serikali tatu
ni wengi lakini kinachofanywa na wanaotaka serikali mbili ni kupotosha
ukweli.
Haji alitolea mfano katika uchaguzi mkuu
wa mwaka 2010, kuwa walioandikishwa kupiga kura walikuwa ni watu 20
milioni, waliopiga kura ni watu milioni nane na ambao walimchagua Rais
Jakaya Kikwete ni watu milioni sita hivyo kwa hoja ya wanaCCM kuhusu
Rasimu ina maana watu 14 milioni hawamtaki Rais Kikwete.
Akizungumzia gharama za Muungano, alisema
fedha nyingi zaidi ya asilimia 70 za Muungano, zinatumika katika
kuendesha Serikali ya Tanganyika jambo ambalo siyo sahihi.
Huku akitoa takwimu mbalimbali, alisema
kwa maana hiyo uchangiaji wa Muungano kamwe hauwezi kuwa sawa kwa pande
zote. “Katika jambo moja tu la askari polisi, tafiti za kimataifa
zinaonesha kuwa askari mmoja anafaa kulinda watu 400, kwa Zanzibar yenye
watu 1.3 milioni inahitaji askari 3,000 tu, lakini Tanganyika yenye
watu zaidi ya 40 milioni inahitaji zaidi ya askari 120,000 hivyo
uchangiaji wa Muungano hauwezi kuwa sawa,” alisema.
Haji pia alieleza kuwa, hati za Muungano
ambazo waliowengi wanasema zinamsingi wa serikali mbili, siyo kweli bali
hati hizo zinatambua serikali tatu, ikiwapo ya Tanganyika.
Hata hivyo, alisema msingi wa serikali
mbili ni mkakati wa CCM ambao ulianza tangu enzi za TANU mwaka 1977,
kutaka kuwa na serikali moja na hivyo, kuifanya Zanzibar kuwa siyo nchi.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment