MAAFISA wa polisi mjini Nyahururu nchini Kenya usiku wa kuamkia Alhamisi walitibua mpango wa watu wasiojulikana wakionya jamii ya waislamu kuhama mjini humo.
Kulingana na mkuu wa polisi Nyandarua kaskazini Benjamin Onsongo, karatasi Zenye ujumbe wa kuwataka Waislamu waondoke mjini humo zilianza kusambazwa Jumapili iliyopita.
Onsongo alisema ilani hiyo iliipa jamii hiyo makataa ya siku saba kuhama mji huo kwani wamekataa kutambulisha maadui wanaoivamia nchi ya Kenya.
“Tumeanzisha uchunguzi na tumewaongeza maafisa wa polisi wanaoshika doria katika eneo hilo na nina uhakika kuwa tutawatia mbaroni wahusika,” alisema Bw Onsongo.
Viongozi wa kiislamu wakiongozwa na Imam wa msikiti wa Jamia mjini Nyahururu Sheikh Mohamed Huka pamoja na mwenyekiti wa muungano wa Waislamu kaunti ya Laikipia Sheikh Isaack Osman waliambia jamii ya waislamu mjini humu kutoogopeshwa na ilani hizo kwani maafisa wa polisi wanalishughlikia suala hilo.
Sheikh Mohamed Huka wa msikiti wa Jamia, Nyahururu akiwa na moja
ya vijikaratasi vilivyosambazwa mji wa Nyahururu Alhamisi vikiwataka watu wa
dini ya Kiislamu wahame mji huo
“Karatasi hizi zinasambazwa na watu wachache ambao wanataka kututawanya kwa misingi ya kidini lakini hatutakubali kugawanywa, ninaamini kuwa Nyahururu ni mji wa amani,” alisema Osman.
Sheikh Huka alisema kuwa jamii ya Waislamu imekubali kukumbatia mfumo wa Nyumba Kumi ili kuinua usalama na kuwauliza kuwa na subira huku maafisa wa polisi wakiendeleza uchunguzi